Habari Kitaifa

Kilimanjaro wapongezwa kwa Kuzindua Mwongozo wa Uwekezaji

on

Mkoa wa Kilimanjaro umepongezwa kwa kuitikia agizo la Rais John Magufuli la kutaka kila mkoa ubainishe fursa za uwekezaji zilizopo na kuandaa mwongozo wa uwekezaji.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais -TAMISEMI, Mhe. Joseph Kakunda katika hafla ya uzinduzi wa mwongozo wa uwekezaji mkoa wa Kilimanjaro uliondaliwa na Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF) kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Akimwakilisha Waziri wa Nchi wa Ofisi hiyo Selemani Jafo, Naibu Waziri huyo alisema kwamba agizo la Rais ambalo limelenga kuweka mikakati mahsusi ya kuipeleka nchi katika uchumi wa viwanda.

Akitoa salamu za pongezi kwa Mkuu wa Mkoa Mh. Anna Mghwira Naibu Waziri Kakunda alisema wakati mkoa wa Kilimanjaro unatekeleza maagizo, serikali kuu nayo inaendelea kuboresha mazingira ya kufanyia biashara ili kuvutia wawekezaji mbalimbali.

Akizungumzia Mwongozo huo Naibu Waziri alisema kwamba kazi ya kubaini fursa za uwekezaji katika miradi mbalimbali yenye faida siyo tu kwa wawekezaji pekee bali pia kwa taifa letu kupitia kodi na upatikanaji wa bidhaa na huduma mbalimbali kwa kila eneo la nchi.

Alisema kazi iliyofanywa na mkoa huo ina maana kubwa kwa kuwa sasa inakuwa rahisi kwa wawekezaji wawe wa ndani au nje kujua namna ya kuwekeza katika mkoa wa Kilimnjaro kwa kuzingatia mahitaji yao na namna rasilimali watu na miundombinu ilivyo.

Alisema agizo la Rais la utengenezaji wa mwongozo unakwenda sanjari na ubainishaji na uandazi wa maeneo ya uwekezaji ili yanapotakiwa yapatikane hima.

Aliutaka mkoa huo kuutangaza mwongozo wao kwani biashara ni matangazo katika maeneo mbalimbali ya kimataifa na ya wawekezaji katika masoko ya hisa kwa njia ya kielektroniki ili wavune utayari wao wa kukaribisha uwekezaji.

Kakunda alisema kwamba mkoa huo kwa asili unaweza kabisa kuvutia wawekezaji. Kinachostahili kufanywa kwa sasa ni kuhakikisha  kauli mbiu ya Kilimanjaro ya Viwanda, inawezekana chukua hatua inatekelezwa kwa vitendo.

Akizungumza kumkaribisha mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Mh. Anna Mghwira alisema kwamba Mwongozo huo utafanyiwa kazi na matunda yake yataonekana wakati taifa linaelekea kwenye uchumi wa viwanda.

Alisema mkoa huo una rasilimali za kutosha kuwezesha wawekezaji mbalimbali kutekeleza adhma ya kuwa na viwanda vidogo na vya kati vinavyotumia rasilimali kutoka mkoani na aliwashukuru wataalam wa ESRF waliowezesha kupatikana kwa muongozo huo na wafadhili ambao ni UNDP.

Naye Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF) Dk Tausi Mbaga Kida  ambayo ndiyo ilipewa jukumu na Mkoa wa Kilimanjaro kufanya utafiti na uchambuzi wa kina ili kubaini fursa za uwekezaji zilizopo katika Mkoa, aliupongeza mkoa wa Kilimanjaro kwa kuona umuhimu wa kuwa na mwongozo wa uwekezaji.

Aidha katika hotuba yake hiyo alisema kuwa taasisi yake ilitengeneza sehemu tatu za taarifa ambazo zote zililenga kutoa uwanda mpana kwa wawekezaji kuwa na taarifa muhimu za uwekezaji katika mkoa wa Kilimanjaro.

Alisema katika hotuba yake kwamba ESRF ilifanikiwa kuandaa ripoti tatu ambazo ni Ripoti ya Fursafiche katika Viwanda (Industrialization Potentials Report), Ripoti ya Fursa za Uwekezaji (Investment Opportunities Report) pamoja na Mwongozo wa Uwekezaji ambao Mkoa umezindua rasmi leo.

Pia alisema kwamba Ripoti hizo zilithibitishwa na Mkoa Oktoba 12, 2017 katika warsha maalum iliyoandaliwa na Mkoa wa Kilimanjaro.

Mapema mwaka huu Mwongozo kama huo ulizinduliwa Mkoani Simiyu ambao umeleta matokeo makubwa ndani ya muda mfupi. Wiki mbili zilizopita mkoa wa Mwanza nao ulizindua mwongozo wa uwekezaji. Mkoa wa Mara katika siku za usoni unatarajiwa kuzindua mwongozo wa uwekezaji. Miongozo yote hiyo imeandaliwa na ESRF.

Alisema miongozo hiyo ya Uwekezaji inaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 na Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016 – 2021) unaosisitiza ujenzi wa Tanzania ya Viwanda ili kuifikisha nchi katika uchumi wa kati ifikapo 2025.

Katika hotuba yake pia Dk Kida aliiushukuru Uongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro chini ya Mkuu wa Mkoa, Anna E. Mghwira, Katibu Tawala wa Mkoa, Mhandisi Aisha S. Amour na viongozi wengine wa mkoa na wilaya zote kwa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wataalamu wakati wanapita kutafuta maoni na alitoa shukurani kwa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa ufadhili wa fedha.

Pia alishukuru timu ya ESRF ikiongozwa na Bi. Margareth Nzuki, Mkuu wa Idara ya Maarifa na Ubunifu kwa kuratibu, watafiti washiriki Prof. Haidari Amani; Dkt. Hoseana Lunogelo na Prof. Samuel Wangwe kwa kupitia mwongozo huu.

About Habari360_TZA

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *